HEADER

Jumatano, 26 Juni 2013

AFRIKA YA KUSINI YAJIANDAA KWA KIFO CHA MZEE NELSON MANDELA


 
SASA kuna kila dalili kuwa taifa la Afrika Kusini, limeanza kujiandaa kukabiliana na tukio zito la kifo cha Rais wa Kwanza wa Taifa hilo, Nelson Mandela (94), ambaye amelazwa kwa siku 18 hospitalini akisumbuliwa na maradhi ya mapafu. Kauli tofauti kuhusiana na mwenendo wa hali ya afya yake na matukio mbalimbali yasiyokuwa ya kawaida yanayoripotiwa kufanywa na familia yake, ndiyo ambayo yameamsha hisia hizo.
 
Taarifa zilizopatikana jana kutoka nchini Afrika Kusini, zinaeleza kuwa watu muhimu katika familia ya Mandela, walikutana kwa dharura na kufanya mazungumzo ya faragha katika kijiji alichozaliwa cha Qunu.

Wakati wanafamilia hao wakikutana, msafara wa magari ya kundi jingine la wanafamilia, ulitemb

elea eneo la makaburi ya ukoo wa Mandela.
Eneo hilo la makaburi ya ukoo lipo mita chache kutoka yalipo makazi ya mdogo wake, Morris Mandela, mkabala na nyumba ya Mandela iliyoko kijijini Qunu.

Haikufahamika mara moja mazungumzo ya wanafamilia yalihusu jambo gani, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika Kusini, vililiripoti kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila la Xhosa, wanafamilia hutembelea eneo la maziko iwapo kuna hisia za mmoja wa wanafamilia kufariki dunia na wakati mwingine kufanya tambiko la kimila.

Waliofika eneo la makaburi ni Winnie Madikizela-Mandela ambaye ni mke wa zamani wa Mandela, Waziri wa Utumishi wa Umma, Lindiwe Sisulu na Kiongozi wa chama cha upinzani cha United Democratic Movement, Bantu Holomisa.

Msafara wao ulifika eneo la makaburi jana asubuhi na kulikuwa na taarifa kuwa mtoto wa kike wa Mandela, Makaziwe Mandela, aliitwa eneo hilo.

Waandishi wa habari walizuiliwa kuvuka geti la eneo la makaburi hayo na waliofika nyumbani kwake Qubu, walipigwa marufuku kusogea karibu na nyumba hiyo.

Wanafamilia walioripotiwa kukutana kijijini Qunu ni Mandla Mandela, Thanduxolo Mandela, Ndaba Mandela na Ndileka Mandela na Chifu Bhovulengwe wa Baraza la AbaThembu.

Kikao hicho kinaeleza kuketi kuanzia saa nne asubuhi, lakini baadhi ya wanafamilia waliotakiwa kukihudhuria walichelewa kwa sababu ya kutopata taarifa mapema.

Familia yake yatoweka hospitali

Taarifa zinaeleza kuwa jana hakuna ndugu wa Mandela aliyeonekana katika hospitali aliyolazwa, isipokuwa timu ya madaktari wake ambayo iliwasili majira ya saa mbili asubuhi.

Kutokuonekana kwa wanafamilia hao hospitalini hapo, kulitafasiriwa kuwa ni kutokana na kikao kilichoitishwa Qunu. Napilisi Mandela, ambaye ni kiongozi wa familia hiyo, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwa familia ya Mandela inakutana kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu afya ya mzee huyo.

Hata hivyo, Napilisi Mandela, alieleza kikao hicho cha kifamilia kinahusu mambo ya kimila na aliyekabidhiwa jukumu la kukiratibu ni Silumko Mandela.

Obama kutomuona

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa Rais wa Marekani, Barack Obama hatamtembelea Mzee Mandela hospitalini alikolazwa mjini Pretoria, kwa sababu hakupangiwa kwenye ratiba yake.

Ratiba ya Obama iliyotangazwa wakati wa ziara yake nchini Afrika ya Kusini, inaonyesha kuwa atatembelea Kisiwa cha Robben ambako Mandela alifungwa wakati wa harakati zake za kupigania uhuru.

Pia atatembelea mji maarufu wa weusi wa Soweto na Chuo Kikuu cha Cape Town, jijini Cape Town.

Daktari wake alonga

Timu ya madaktari wanaomtibu, jana ilitoa taarifa kuwa hali yake haijabadilika.

Rais Zuma awatuliza Waafrika Kusini

Rais Jacob Zuma amelihutubia taifa kwa njia ya televisheni na kueleza kuwa hali ya Mzee Mandela inaridhisha, huku akieleza pia kuwa maendeleo ya afya yake hayafahamiki.

Zuma alisema hawezi kujua kama Mandela yuko kwenye hali mbaya, kwa sababu yeye hajui mtu anayekuwa katika hali hiyo anakuwaje, hivyo wenye nafasi ya kuzungumzia suala hilo ni madaktari wake wanaomtibu.

Katika hotuba yake alisema hali ya Mandela imekuwa ikibadilika badilika kila baada ya saa 24, hivyo ni jambo gumu kujua kinachokuja mbele.

Zuma alimtembelea Mandela Jumapili akiwa ameambatana na Makamu wa Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...